• DRC yasisitiza kuwa uchaguzi wa rais utafanyika mwaka huu kama ulivyopangwa

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema uchaguzi wa rais utafanyika mwishoni mwa mwaka huu kama ulivyopangwa licha ya changamoto wanazokabiliwa nazo.

Katika mahojiano na shirika la habari la Reuters, Bruno Tshibala amesema uchaguzi huo utafanyika Disemba 23 akisisitiza kuwa vyombo husika vipo mbioni kuhakikisha kuwa matayarisho ya zoezi hilo la kidemokrasia yanakamilika kabla ya tarehe hiyo.

Amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini humo CENI inafanya juu chini kuhakikisha kuwa mashine za biometriki zinasaidia pakubwa katika kufanikisha uchaguzi huo.

Kadhalika amebainisha kuwa, serikali ya nchi hiyo haitasita kuziomba taasisi za kimataifa za fedha kulipiga jeki zoezi hilo, akisisitiza kwamba kwa sasa serikali inakabiliwa na changamoto za kifedha na kilojistiki.

Rais Joseph Kabila

Mwaka uliopita na baada ya CENI kutangaza kuwa uchaguzi ujao wa rais utafanyika Disemba mwaka huu, chama kikuu cha upinzani nchini humo UPDS kilisema hakikubaliana na ratiba hiyo ya uchaguzi, na kile wanachotaka kuona kikifanyika ni Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo kuachia ngazi kabla ya uchaguzi wenyewe.

Viongozi wa upinzani na wa Kanisa Katoliki nchini Kongo DR wamekuwa wakiwataka wananchi washiriki kwa wingi katika maandamano ya amani ya kutaka kutamatishwa miaka 17 ya utawala wa Kabila.

Tags

Mar 08, 2018 16:09 UTC
Maoni