Mar 19, 2018 08:08 UTC
  • Profesa Lipumba: Chama cha CUF kimemdekeza sana Maalim Seif, Mazrui amjibu

Mwenyekiti wa chama cha CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba amesema kuwa, chama hicho kilimdekeza kwa kiasi kikubwa Katibu mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad.

Kwa mujibu wa Lipumba hali hiyo imesababisha chama hicho kushindwa kupata viongozi watakaoingia katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar sambamba na kutokuwepo kwake kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Lipumba alitoa kauli hiyo Jumapili ya jana wakati akifungua kikao cha kwanza cha kawaida cha Baraza Kuu la Uongozi wa CUF kinachofanyika makao makuu ya chama hicho, Buguruni jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Mahasimu wawili wa kisiasa ambao zamani walikuwa pamoja

“CUF tumemdekeza kwa muda mrefu na zile nyimbo tulizokuwa tukiimba ya kuwa akipata Seif tumepata sote zilikuwa zimemuingia kichwani kwelikweli na yeye alitafsiri kuwa akikosa Seif tumekosa sote,” alisema Profesa Lipumba. Kufuatia kauli hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar ambaye yupo upande wa Maalim Seif, Nassor Ahmed Mazrui amesema chama hicho hakijamdekeza katibu huyo, bali kinaringia kura anazopata kila anapowania urais visiwani Zanzibar. Katika ufafanuzi wake, Mazrui amesema Maalim Seif anabebwa na kura za urais wa Zanzibar na wananchi wameonyesha wazi kumpenda na kumkubali.

Nassor Ahmed Mazrui,Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar ambaye yupo upande wa Maalim Seif

Katika sehemu nyingine Lipumba amesema kuwa, ziara yake ya hivi karibuni Pemba imesaidia kuimarisha chama hicho na hivi sasa wananachi na viongozi wa CUF wanaijua vyema Katiba ya chama tofauti na hapo awali. Awali Maalim Seif Sharif Hamad alitoa radiamali kuhusiana na ziara ya Profesa Lipumba huko Pemba na kusema kuwa, ziara hiyo ilikuwa na lengo la kuibua ghasia na machafuko kati ya wanachama wa CUF ili kutoa mwanya kwa msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania kukifuta chama hicho.

Tags

Maoni