• Seif al-Islam Gaddafi ajiandikisha kugombea urais nchini Libya

Mkuu wa Mipango ya Mwana wa Kanali Muammar Gaddafi, yaani Seif al-Islam Gaddafi ametangaza kuwa, mwana huyo wa kiongozi wa zamani wa Libya ameandikisha jina lake la kuwa miongoni mwa wagombea katika uchaguzi ujao wa rais nchini humo.

Aiman Bouras ameyasema hayo akiwa nchini Tunisia na kuongeza kuwa, lengo la Seif al-Islam kugombea uchaguzi huo, si kulipiza kisasi na wala si uchu wa madaraka. Bouras amedai kwamba, mwana huyo wa Kanali Muammar Gaddafi ana ratiba ya kila upande na kamili yenye nyanja tofauti za kisiasa, kiusalama na kijamii kwa ajili ya Libya.

Wakati Seif al-Islam Gaddafi alipokuwa akishikiliwa jela

Aiman Bouras amesema kuwa, Seif al-Islam Gaddafi kwa sasa yuko nchini Libya na yupo huru na kwamba muda si mrefu atadhihiri kati ya wananchi. Hii ni katika hali ambayo awali Jenerali Khalifa Haftar alinukuliwa akisema kuwa, Seif al-Islam anashikiliwa katika moja ya jela za Libya. Itakumbukwa kuwa, miaka michache tangu alipouawa baba yake, Kanali Muammar Gaddafi, Seif al Islam alitiwa mbaroni na kuendelea kusalia jela nchini Libya hadi mwezi Juni mwaka jana ilitangazwa kwamba amepata msamaha na kuachiliwa huru.

Kanali Muammar Gaddafi, aliyekuwa kiongozi wa Libya

Hayo yanajiri huku baraza la wawakilishi nchini Libya likiwa limeonya mara kadhaa juu ya suala la kuachiliwa huru bila masharti yoyote viongozi wa utawala uliopita, wa Muammar Gaddafi, aliyeuawa mwaka 2011 kufuatia mapinduzi ya wananchi na kadhalika uingiliaji wa madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani.

Tags

Mar 20, 2018 08:01 UTC
Maoni