• Human Rights Watch yatoa wito wa kufanyika uchaguzi huru Libya

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limewataka viongozi wa Libya kuchukua hatua madhubuti ili kudhamini uchaguzi huru na wa haki katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Taarifa ya Human Rights Watch iliyotolewa leo imeeleza kwamba, uchaguzi ujao nchini Libya unapaswa kufanyika katika mazingiya yasiyo ya kibaguzi, kulazimisha, ingawa ni jambo gumu kuandaliwa mazingira hayo baada ya matukio ya mwaka 2011.

Sambamba na kusisitiza juu ya kuheshimiwa uhuru wa kutoa maoni, kuchungwa mamlaka ya Katiba na kuweko anga huru kwa ajili ya kila mtu aliyetimiza masharti kuweza kushiriki katika uchaguzi huo, shirika la Human Rights Watch limeeleza kwamba, kuna haja ya kuweko chombo cha mahakama chenye utendaji mzuri ambacho kitaweza kushuhughulikia kwa uadilifu malalamiko yatakatojitokeza baada ya uchaguzi Libya.

Machafuko ya Libya

Eric Goldstein, Naibu Mkuu wa Human Rights Watch kanda ya Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika amesema kuwa, Libya ya leo iko mbali  mno na suala la kuheshimiwa mamlaka ya sheria, haki za binadamu na kuwa na mazingira yenye kukubalika kwa ajili ya kufanyika uchaguzi huru.

Libya ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa na hali ya mchafukoge tangu kupinduliwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011, kufuatia uingiliaji kijeshi wa Marekani na waitifaki wake katika Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato).

Tags

Mar 21, 2018 14:14 UTC
Maoni