Apr 19, 2018 15:10 UTC
  • Ukosefu wa usalama wakwamisha shughuli za masomo kaskazini mwa Kenya

Ukosefu wa usalama katika Kaunti ya Wajir nchini Kenya unaelezwa kuwa unatishia kuvuruga shughuli za masomo katika shule nyingi za maeneo hayo.

Ripoti zaidi zinasema kuwa, walimu wengi wameomba kuhamishwa kutoka eneo hilo kufuatia visa vya kuuawa kwa walimu watatu mwezi Februari na washambuliaji wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabab.

Walimu wanaotoroka katika maeneo hayo ya kaskazini mwa Kenya wanadai kwamba, wenzao waliuawa kwa misingi ya kidini. Inaelezwa kuwa, tatizo hilo limeonekana kushadidi zaidi katika miaka mitatu ya hivi karibuni.

Katika shule ya Sekondari ya Wajir, wanafunzi wa kidato cha tatu wanafanya mtihani, ilihali hakukuwa na masomo yaliyofundishwa kwa sehemu kubwa ya muhula huu hali ambayo inatishia kufanya vizuri wanafunzi hao katika mtihani.

Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Wajir

Shule hiyo ina upungufu wa walimu kumi na sita. Walimu wanane wa shule hiyo  walitoroka hivi majuzi baada ya walimu watatu kuuawa katika shule moja inayopakana na Somalia.

Wanafunzi wamelazimika kujifunza wenyewe, jambo ambalo linamtia wasiwasi Mohammed Shukri, anayejiandaa kufanya mtihani wake wa kufuzu kujiunga na chuo kikuu mwishoni mwa mwaka.

'Tuna wasiwasi wa matokeo baada ya mtihani. Na unajua kwamba mwisho wa mwaka tutakuwa tunafanya mtihani sawa na wanafunzi wengine kote nchini, ambao wana walimu wa kuwafunza shuleni', amesema Mohammed Shukri.

Inasemekana kuwa, walimu walianza kulikimbia eneo hilo mwaka 2015, kufuatia mauaji ya zaidi ya wanafunzi 140 katika Chuo Kikuu cha Garissa.

Tags

Maoni