Mei 23, 2018 02:45 UTC
  • Kikao cha majirani wa Libya nchini Algeria

Nchi zinazopakana na Libya zimeitisha kikao huko Algeria kwa ajili ya kuchungua mgogoro wa nchi hiyo na kutafuta njia za kuyakutanisha pamoja makundi mbalimbali kwa ajili ya kuleta umoja wa kitaifa nchini Libya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Abdelkader Messahel, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Sameh Shoukry na  Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia, Khamis al Jahnawi, wamekutana mjini Algiers na kujadiliana matukio ya hivi karibuni kabisa ya kisiasa na kiusalama ya nchini Libya. Sabamba na kufanyika kio hicho, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nalo limeitisha kikao kuhusu Libya ambapo Ghassan Salamé, mjumbe maalumu wa umoja huo nchini humo amewasilisha ripoti yake mbele ya baraza hilo la usalama. 

Vikao hivyo vimefanyika katika hali ambayo, mazingira ya kisiasa ya Libya na mashaka yanayotokana na mazingira hayo yanaendelea kuleta matatizo mengi si ndani ya Libya tu, bali pia kwa nchi zinazopakana nayo. Magenge ya kigaidi, wahajiri haramu, magenge ya magendo ya silaha na binadamu mipakani na matatizo mengine chungu nzima, ni miongoni mwa mambo yanayozitia wasiwasi nchi zinazopakana na Libya. 

Mawaziri wa mambo ya nje wa Algeria, Tunisia na Misri

Kwa muda sasa suala la kufanyika uchaguzi na kuundwa serikali kuu yenye nguvu ambayo itaweza kudhibiti hali ya mambo nchini humo limekuwa likifuatiliwa kwa nguvu zote duniani kwani ndiyo njia kuu ambayo jamii ya kimataifa inaamini inaweza kutatua mgogoro wa Libya. Viongozi wa Libya wameshakubaliana na suala la kufanyika uchaguzi nchini humo. Hata hivyo tatizo lililopo ni kuhusu tarehe na namna ya kufanyika uchaguzi wenyewe.

Ahmed Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amesema kuhusu wajibu wa kufanyika uchaguzi nchini Libya kabla ya kumalizika mwaka huu wa 2018 kwamba: Iwapo juhudi za kuitisha uchaguzi huo zitashindwa, basi mgogoro wa Libya utazidi kuwa mkubwa.

Amma tatizo kubwa zaidi lililoko nchini Libya hivi sasa ni kuenea silaha mikononi mwa makundi yenye malengo, shabaha, maslahi na itikadi tofauti. Tatizo jingine kubwa ni uingiliaji wa siri na wa dhahiri wa mikono ya nje katika masuala ya ndani ya Libya. Mambo kama hayo ndiyo yanayokwamisha juhudi za kuitisha uchaguzi, kuunda serikali kuu yenye nguvu na kudhibiti hali ya mambo nchini Libya. Pamoja na kwamba viongozi wa nchi hiyo wamekubali kuitishwa uchaguzi, lakini wanasema hawakubaliani na mipango na mbinu zilizopendekezwa na madola ajinabi za kuendesha uchaguzi huo. Bali wanasema mbinu za namna ya kuitisha uchaguzi huo lazima zipangwe na kuamuliwa na Walibya wenyewe. 

Uingiliaji wa madola ajinabi kama Imarati hauruhusu kupatikana amani na utulivu nchini Libya

Abdullah Balhiq, msemaji wa Bunge la Tobruk la mashariki mwa Libya amesema, utatuzi wa mgogoro wa Libya utaletwa na wananchi wenyewe wa Libya na si nchi ajinabi.

Pamoja na hayo, bado nchi ajinabi zikiwemo za Kiarabu kama Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) zinaendelea kuingilia mambo ya ndani ya Libya, suala ambalo haliangaliwi kwa sura nzuri hata kidogo na viongozi wa nchi hiyo. Isa Tuwaijir, waziri wa zamani wa mipango wa Libya amesema: Mgogoro wa Libya utaweza kutatuliwa iwapo tu Waimarati wataacha kuingilia masuala ya ndani ya nchi yetu.

Hata hivi sasa na ijapokuwa kunafanyika vikao kwa lengo la kusaidia kutatua mgogoro wa Libya, lakini wachambuzi wa mambo wanasema, kuitisha vikao kama hivyo tu hakutosaidia kitu. Mtazamo wa wachambuzi hao ni kwamba utatuzi wa kweli wa mgogoro wa Libya utapatikana kupitia mshikamano wa taifa hilo zima kwani ni kwa mshikamano huo wa matabaka yote ya wananchi wa Libya ndipo wataweza kukabiliana na vishawishi vyote vya ndani na nje na hatimaye kuleta utulivu na amani ya kudumu nchini mwao.

Tags

Maoni