Mei 23, 2018 03:37 UTC
  • Wakazi wa mashariki mwa Kongo waandamana kulaani udhaifu wa jeshi katika kukabiliana na waasi

Utendaji dhaifu wa jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika kukabiliana na waasi wa maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo, umewakasirisha wakazi wa maeneo hayo na kuamua kufanya maandamano.

Wakazi wa maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo sambamba na kulalamikia mashambulizi ya watu wenye silaha katika mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wamelituhumu jeshi la nchi hiyo kwa kuchelewa kuchukua hatua za maana katika kukabiliana na waasi. Kwa mujibu wa wakazi wa mashariki mwa Kongo DR, askari wa serikali hawana uwezo wa kudhamini usalama wa maeneo hayo. Hivi karibuni raia 10 walishambuliwa na kuuuawa na waasi wenye mafungamano na kundi la waasi wa Uganda ADF mjini Beni, mkoa wa Kivu Kaskazini.

Baadhi ya wanamgambo wanaofanya mauaji maeneo ya mashariki mwa Kongo DR

Waasi wa Uganda wamekuwa wakiendesha shughuli zao katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo ya katikati mwa Afrika tangu mwaka 1994 na katika kipindi hicho mamia ya watu wameuawa na wengine wengi kuachwa vilema hususan eneo la Beni. Maeneo ya katikati, mashariki na kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamekuwa yakishuhudia machafuko kwa miaka 20 sasa. Kushindwa jeshi la nchi hiyo na lile la kusimamia amani la Umoja wa Mataifa katika kukabiliana na makundi ya wanamgambo, kunatajwa kuwa chanzo cha ongezeko la machafuko katika maeneo hayo.

Tags

Maoni