Mei 24, 2018 04:09 UTC
  • Umoja wa Afrika waitisha mkutano kujadili mgogoro wa mpakani wa Sudan na Sudan Kusini

Umoja wa Afrika utafanya mkutano kati ya Sudan na Sudan Kusini kwa lengo la kutatua mgogoro kuhusu eneo la mpakani la Abyei.

Mkuu wa kamati ya usimamizi wa pamoja ya Abyei AJOC kwa upande wa Sudan Bw. Hassan Ali Nimir amesema, wamepata mwaliko kutoka Umoja wa Afrika kuhudhuria mkutano wa kamati hiyo uliopangwa kufanyika tarehe 30 mwezi huu wa Mei. Pia amesema, mkutano huo utafanyika kwa siku mbili na utahudhuriwa na viongozi wa utawala wa asili wa makabilia ya Dinka Ngok na Messiria.

Umoja huo unazipatanisha Sudan na Sudan Kusini juu ya eneo la Abyei lenye utajiri wa mafuta, ambalo lipo mpakani, na nchi hizo mbili zote linadai kulimiliki. Eneo hilo linakaliwa na kabila la Dinka Ngok la Sudan Kusini na kabila la Arab Messiria la Sudan.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini (kushoto) na Rais Omar Bashir wa Sudan

Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 kwa kupiga kura ya maoni iliyoungwa mkono na asilimia 99 ya raia wake baada ya vita vya miongo kadhaa vya kutaka uhuru. Inasadikiwa kuwa Sudan Kusini ilichochewa na madola ya kibeberu kujitenga na Sudan.

Vita vya ndani nchini humo vilivanza Disemba 2013 na vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.

Tags

Maoni