Mei 24, 2018 14:50 UTC
  • Wanadiplomasia wawili wa Angola waachishwa kazi kwa kuhudhuria dhifa ya ufunguzi wa ubalozi wa US Quds

Serikali ya Angola imewaachisha kazi wanadiplomasia wake wawili waandamizi kwa kuhudhuria dhifa ya kusherehekea ufunguzi wa ubalozi wa Marekani katika mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu iliyofanyika tarehe 13 Mei.

Manuel Augusto Jao Diogo Fortunato, mwanadiplomasia namba mbili katika ubalozi wa Angola mjini Tel Aviv ameachishwa kazi kwa kuhudhuria sherehe hiyo; naye Joaquim do Espirito Santo, Mkurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Angola anayehusika na masuala ya Jumuiya za Afrika na Mashariki ya Kati, amepigwa kalamu nyekundu pia kwa kumpa idhini Fortunato ya kufanya hivyo.

Gazeti rasmi la serikali ya Angola limeripoti kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Manuel Augusto amewaachisha kazi wanadiplomasia hao wawili kwa kushindwa kuheshimu taratibu na kwa kuitia doa sura na jina zuri la Angola.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola,  Manuel Augusto

Fortunato alikuwa mmoja wa wanadiplomasia 12 wa nchi za Afrika waliohudhuria dhifa ya chakula cha usiku ya kusherehekea ufunguzi wa ubalozi wa Marekani katika mji wa Quds, wakiwemo pia wanadiplomasia kutoka Rwanda, Sudan Kusini, Kenya, Ethiopia, Ivory Coast, Cameroon na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Huko nyuma pia Angola ilichukua msimamo dhidi ya sera za kujipanua za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ilipounga mkono azimio la Desemba mwaka 2016 lililopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani ujenzi wa vitongoji unaofanywa na utawala huo ghasibu katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.

Inafaa kuashiria kuwa hatua ya baadhi ya nchi za Afrika ya kuhudhuria sherehe ya ufunguzi wa ubalozi wa Marekani huko Baitul Muqaddas imelaaniwa na kukosolewa vikali na wanaharakati mbalimbali barani humo.

Julius Malema, kiongozi wa chama cha EFF nchini Afrika Kusini

Julius Malema, mbunge na kiongozi wa chama Wapigania Uhuru wa Kiuchumi (EFF) nchini Afrika Kusini amesema, kitendo hicho ni usaliti wa upeo wa juu kabisa kwa sababu wakiwa ni Waafrika, nchi hizo zingepaswa kujua kwamba ukoloni na ubeberu havina nafasi katika utu na ubinadamu.../

Tags

Maoni