Mei 25, 2018 07:32 UTC
  • AU, UN na IGAD zataka kusitishwa mapigano kati ya Puntland na Somaliland

Jamii ya kimataifa imeeleza juu ya wasi wasi mkubwa ilionao kutokana na kushtadi mapigano kati ya vikosi vya maeneo yenye mamlaka ya ndani ya Somaliland na Puntland nchini Somalia.

Umoja wa Afrika AU, Umoja wa Mataifa UN, Umoja wa Ulaya EU na Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya Nchi za Afrika Mashariki IGAD zimetoa taarifa katika nyakati tofauti kulaani mapigano hayo huku zikitaka pande husika kusitisha mapigano hayo mara moja;

Mwito huo umetolewa baada ya kuripotiwa mapigano mapya katika eneo hilo jana asubuhi, ambapo silaha nzito zilitumiwa na askari wa pande hasimu.

Taarifa za asasi hizo za kimataifa zimewataka makanda wa maeneo hayo mawili yenye mamlaka ya ndani nchini Somalia kuandaa mazingira ya kufanyika mazungumzo ya kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo.

Aidha wamezitaka pande husika katika mgogoro huo kuruhusu kupelekewa misaada na huduma za kibinadamu watu walilazimika kuyaacha makazi yao kutokana na vita hivyo.

Hali duni ya maisha katika wilaya ya Tukaraq, mpakani mwa Puntland na Somaliland

Zaidi ya watu 50 wameuawa kwenye mapigano hayo, huku Rais wa Somaliland, Muse Bihi Abdi akitangaza kuwa jeshi lao limeshinda kwenye vita hivyo huku akiilaumu serikali ya Somaliland kwa kuanzisha 'uvamizi wa wazi' dhidi ya utawala wake.

Siku chache kabla ya kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani, Rais Mohammed Abdullahi Farmajo wa Somalia alitoa taarifa ya kulaani mapigano hayo na kusema "Ni jambo la kusikitisha sana kumwaga damu wakati huu tunapojiandaa kwa mwezi mutukufu wa Ramadhani, pande husika kwenye mgogoro huo zinapaswa kusitisha mapigano hayo mara moja na bila masharti yoyote, na wautafutie ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo."

Tags

Maoni