Mei 25, 2018 13:43 UTC
  • WHO: Tanzania ipo nafasi ya pili ya hatari kukumbwa na ugonjwa hatari wa Ebola

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeitaja Tanzania kuwa ipo na nafasi ya pili ya nchi zilizo katika hatari ya kukumbwa na maambukizi ya ugonjwa hatari wa Ebola.

Hali hiyo imetokana na uwepo wa maingiliano ya kibiashara, kijamii na kiuchumi kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Tanzania. Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Shirika la Afya Duniani, Tanzania inashika nafasi ya pili baada ya Kongo Brazzaville ambayo ipo katika kundi la kwanza.

Bendera ya Tanzania

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa, mwakilishi wa shirika hilo nchini Uganda, Dk Miriam Nanyunja amesema kuwa, WHO imeziweka nchi katika makundi matatu kwa kuzingatia nchi ya Congo DR yenye mwingiliano mkubwa na nchi zinazoizunguka. Aidha amesema kuwa, taifa hilo la katikati mwa Afrika limekuwa maingiliano ya usafirishaji, watu kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kukua kwa huduma za kiafya baina ya nchi moja na nyingine.

Dk Miriam Nanyunja, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani WHO

Kwa msingi huo ameitaja Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa iliyo kundi la pili la hatari ya kukumbwa na janga hilo huku ikifuatiwa na Angola, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini na Zambia. Aidha Nanyunja amefafanua kuwa, nchi iliyo katika kundi la tatu ni Uganda, ambapo ipo kwenye hatari lakini kwa kuzingatia kuwa taifa hilo liliwahi kuwa na wagonjwa wa Ebola hapo nyuma, hivyo wana uwezo wa kukabiliana na maradhi hayo ikilinganishwa na nchi nyingine.

Tags

Maoni