Mei 26, 2018 02:22 UTC
  • Gutteres: Dunia iunge mkono azma ya Afrika yenye amani na ustawi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ametoa wito kwa dunia kuunga mkono nchi za Afrika ili ziweze kupiga hatua zaidi katika ustawi na maendeleo.

Ijumaa Mei 25 ilikuwa ni Siku ya Afrika ikiwa ni maadhimisho ya miaka 55 tokea uanzishwe Umoja wa nchi huru za Afrika, OAU ambao sasa ni Muungano wa Afrika, AU.

Akizungumzia siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema kama ambavyo jina limebadilika, vivyo hivyo hali ya bara la Afrika.

Amesema hivi sasa kuna mafanikio makubwa barani Afrika akitolea mfano uzinduzi wa hivi karibuni wa eneo la soko huru barani humo na kusema litatochea ukuaji wa kiuchumi kwa wakazi bilioni 1.2 wa bara hilo na hatimaye kutokomeza umaskini.

Aidha amegusia kasi ya ukuaji wa ujasiriamali, idadi ya watoto wanaopata elimu pamoja na kupungua kwa vifo vya watoto wachanga huku wanawake wengi zaidi wakichaguliwa kuwakilisha jamii zao kwenye mabunge.

Guterres amesema kwa sasa Afrika inazidi kuongeza kasi ya kujiendeleza kwa kuzingatia dira yake ya maendeleo ya mwaka 2063 huku akisisitiza umuhimu wa amani barani humo ili kufanikisha malengo hayo ya muda mrefu.

Hali kadhalika Guterres amesema Umoja wa Mataifa utashirikiana na AU kusaidia mpango wake wa kuhakikisha mapigano barani humo yanasitishwa ifikapo mwaka 2020. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameendelea kusema kuwa “katika siku hii ya Afrika, nasihi mataifa yote yaunge mkono azma ya Afrika yenye amani na ustawi. Kilicho bora kwa Afrika ni bora kwa dunia nzima.”

 

Tags

Maoni