• Mahakama ya Katiba Madagascar yaagiza kuundwa serikali ya muungano

Mahakama ya Katiba nchini Madagascar imemuagiza Rais Hery Rajaonarimampianina wa nchi hiyo kuvunja serikali ya sasa na kuunda serikali ya muungano, kwa lengo la kutamatisha mgogoro wa kisiasa unaoshuhudiwa katika kisiwa hicho kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Mahakama hiyo ilitoa agizo hilo jana Ijumaa na kubainisha kuwa, serikali ijayo ya muungano wa kitaifa na ambayo itajumuisha Waziri Mkuu atakayekubaliwa na pande zote hasimu za kisiasa, iundwe ndani ya siku saba zijazo.

Mahakama hiyo imefafanua kuwa, uundwaji wa serikali hiyo uendane na matokeo ya uchaguzi wa mwisho wa Bunge, na kwamba serikali hiyo ya muungano itatwikwa jukumu la kuandaa uchaguzi wa mapema ambao unapaswa kufanyika kati ya sasa na mwezi Septemba mwaka huu.  

Mapema mwezi huu, mahakama hiyo ya katiba katika kile kilichoonekana ni kujaribu kushusha joto la kisiasa na kupunguza ghadhabu za waandamanaji, ilitangaza kufuta baadhi ya sheria mpya za uchaguzi zinazopingwa na wapinzani.

Maafisa usalama wakikabiliana na waandamanaji

Tangu tarehe 21 Aprili, wapinzani wa Rais Rajaonarimampianina wamekuwa wakifanya maandamano wakitaka kubatilishwa sheria za uchaguzi zilizopasishwa hivi karibuni ambazo walizitaja kuwa na upendeleo, sanjari na kumtaka rais huyo ajiuzulu.

Marc Ravalomanana aliyewahi kuwa rais wa Madagascar anashirikiana na aliyemrithi kiti hicho, Andy Rajoelina, kupinga marekebisho na sheria hizo mpya za uchaguzi.

Mei 26, 2018 07:59 UTC
Maoni