Jun 24, 2018 01:14 UTC
  • Harakati ya mitandao ya kijamii ya kumtaka Rais Sisi wa Misri aondoke madarakani

Kufuatia kuendelea kuwa mbaya mgogoro wa kiuchumi na kisiasa nchini Misri, wananchi ambao wanakandamizwa sasa wameamua kutumia mitandao ya kijamii hasa Twitter kulalamikia utawala wa Rais Abdel Fatah el Sisi huku wengi wakimtaka aondoke madarakani.

Taarifa zinasema watumizi wa mitandao ya kijamii wanatumia hashtegi ya Kiarabu yenye maana ya 'Ondoka Ewe Sisi' ikiwa ni njia ya kulalamikia sera za kiuchumi za Rais Abdel Fataha el Sisi wa nchi hiyo.

Wamisri wanalalamikia vikali uamuzi wa hivi karibuni wa serikali hasa kuondolewa ruzuku na kupandishwa bei ya mafuta ya petroli na ongozeko la bei ya bidhaa muhimu za kila siku.

Taarifa zinadokeza kuwa hasira zimeenea kote Misri ambapo wananchi wanasema hawawezi kustahamili tena ughali wa maisha.

Wananchi wa Misri pia wanalalamikia ukandamizaji mkubwa unaotekelezwa na serikali ya el-Sisi ambayo inapata uungaji mkono wa jeshi na pia madola ya magharibi hasa Marekani. 

Itakumbukwa kuwa mwezi Juni 2013, Muhammad Mursi, rais wa kwanza kuchaguliwa kwa njia ya demokrasia Misri kutoka harakati ya Ikhwanul Muslimin, aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Jenerali el-Sisi wa nchi hiyo. Mursi aliingia madarakani kupitia uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Juni mwaka 2012 na baada ya kutimuliwa madarakani diktetea wa muda mrefu wa nchi hiyo Husni Mubarak.

El-Sisi alishiriki katika uchaguzi uliofuata na kuchaguliwa ambapo baada ya hapo amewakandamiza wapinzani ikiwa ni pamoja na kuipiga marufuku Harakati ya Ikwanul Muslimin na kumfunga jela Mursi pamoja na idadi kubwa ya wafuasi wa harakati hiyo. Mwezi Machi el-Sisi alichaguliwa kwa muhula wa pili  kwa asilimia 92 ya kura ambapo harakati ya Ikhwanul Muslimin ilipigwa marufuku na kuzuiwa kushiriki uchaguzi huo.

Tags

Maoni