Jul 12, 2018 14:56 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Ndani Tanzania: Sakata la wahamiaji haramu uhamiaji ijitathimini

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Kangi Lugola ameitaka idara ya Uhamiaji kujitathmini kuhusiana na suala la wahamiaji haramu ambao wamekuwa wakiingia nchi hiyo mara kwa mara.

Akizungumza katika kikao cha watendaji wakuu wa Idara ya Uhamiaji baada ya kutembelea makao makuu ya idara hiyo, Lugola amewataka askari wa uhamiaji waliopo katika maeneo ya mpaka kujitafakari kutokana na kile alichokisema kuwa utendaji wao hauridhishi. Amesema kuwa ametoa kauli hiyo kutokana na ongezeko la wahamiaji haramu wanaoingia nchini Tanzania kukipitia maeneo ya mipakani.

Wahamiaji haramu ambao wamekuwa wakinaswa nchini Tanzania wakijaribu kuvuka mpaka kwenda nchi nyingine

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania ameongeza kuwa, ni ajabu kuona wahamiaji hao wakipakiwa katika magari na kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine bila hata kukamatwa. “Tatizo liko wapi, inakuaje magari yaliyobeba wahamiaji yanatokea mpaka wa Himo (Kilimanjaro), yanapita Arusha na Manyara yanakwenda kukamatiwa Dodoma?”, amehoji kiongozi huyo wa serikali. “Uhamiaji mnakuwa wapi? Inasikitisha watu hawa wanapita mikoa hiyo bila kukamatwa. Amewataka watu wa mipakani wajitafakari sana na kwamba hali hiyo haikubaliki.”

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania amemtaka Anna Makakala, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, kutowatetea askari wasiotekeleza majukumu yao kwa ufanisi sambamba na kuzuia rushwa kwa wafanyakazi wa  idara tajwa.

Waziri Kangi Lugola, akimuaga Anna Makakala, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji kulia

Katika sehemu nyingine Kangi Lugola ameahidi kuwakimbiza watendaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa lengo la kuwaona wanafanya kazi kwa ufanisi. Amebainisha kwamba anafanya hivyo kwa kuwa wizara hiyo haijasemwa vizuri na Rais John Magufuli wa Tanzania. 

Tags

Maoni