Jul 12, 2018 15:00 UTC
  • Sudan yamwita balozi wa EU kulalamikia matamshi ya kutiwa mbaroni al Bashir

Kufuatia taarifa iliyotolewa na Umoja wa Ulaya juu ya udharura wa kutiwa mbaroni Rais Omar Hassan Ahmad al-Bashir wa Sudan, Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo imemwita balozi wa umoja huo mjini Khartoum na kumfikishia malalamiko yake.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imemwita Jean Michel Dumond, balozi wa EU mjini Khartoum na kumweleza kwamba Khartoum haikuridhishwa na taarifa ya umoja huo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan Qaribullah al-Khadhar amesema kuwa, Abdul Ghani Al Naeem, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa wizara hiyo sambamba na kumwita balozi huyo wa EU, amemweleza kwamba matamshi ya umoja huo yana lengo la kuziwekea mashinikizo nchi za Kiafrika kwa ajili ya kumtia mbaroni Rais Omar al-Bashir.

Inafaa kuashiria kuwa, hivi karibuni Umoja wa Ulaya ulitoa taarifa ukieleza kusikitishwa na hatua za  serikali za Djibouti na Uganda ambazo hivi karibuni zilimkaribisha Rais wa Sudan, kutokana na kushindwa kumtia mbaroni kiongozi huyo.

Jean Michel Dumond, balozi wa EU mjini Khartoum

Mwaka 2009 na 2010, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ilitoa kibali cha kutiwa nguvuni Rais Omar Hassan Ahmad al-Bashir wa Sudan kwa tuhuma za kuhusika na jinai dhidi ya binadamu, vita na kufanya mauaji ya umati katika eneo la Darfur. 

Rais Omar Hassan Ahmad al-Bashir wa Sudan aliingia madarakani mwaka 1989 kwa kufanya mapinduzi dhidi ya Waziri Mkuu wa Wakati huo na kuanzia mwaka 1993 amekuwa akiiongozi nchi hiyo hadi leo.

Tags

Maoni