Jul 18, 2018 13:51 UTC
  • Salva Kiir na Riek Machar kutia saini mkataba wa amani Alkhamisi ya kesho

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan imetangaza kuwa, pande hasimu nchini Sudan Kusini zimefikia makubaliano ya kugawana madaraka ambayo yatatiwa saini Alkhamisi ya kesho.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na hasimu wake, Riek Machar kesho wanatarajiwa kutiana saini makubaliano ya awali ya kugawana madaraka kabla ya mkataba wa mwisho tarehe 26 mwezi huu.

Pande hasimu Sudan Kusini zimeafiki kugawana madaraka kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na pande hizo ambapo kwa mujibu wake kiongozi wa waasi nchini humo, Riek Machar atarejeshwa katika wadhifa wake wa awali wa Makamu wa Rais.

Hivi karibuni Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan ilitangaza kuwa, imeafikiwa kwamba kutakuwepo Makamu wanne wa Rais; yaani Makamu wawili wa Rais waliopo hivi sasa pamoja na Riek Machar, na nafasi ya nne ya Makamu wa rais atapatiwa mwanamama kutoka kambi ya upinzani.

Wakimbizi wa Sudan Kusini

Pande mbili hasimu huko nchini Sudan Kusini zinatuhumiwa kuhusika katika mauaji ya ulipizaji kisasi ambayo yaliibua migawanyiko ya kikabila. Makumi ya maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi kufuatia machafuko hayo.

Nchi hiyo, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake.

Tags

Maoni