• Al-Shabaab yateka mji muhimu katika eneo la Puntland, Somalia

Kundi la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabaab la Somalia limeteka mji mdogo lakini wa kistratajia ulioko karibu na eneo la milima ya Galgala, kusini mwa jiji la Bosaso katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland.

Wakazi wa eneo hilo wamesema mji wa Af Urur, ulioko yapataka kilomita 100 kusini mwa jini la Bosaso kwa sasa uko chini ya udhibiti wa al-Shabaab, na kwamba genge hilo limeuteka leo asubuhi baada ya jeshi la Puntland kuondoka.

Mohamed Abdi, afisa wa jeshi la Puntland amesema mji huo hadi kufikia jana jioni ulikuwa unadhibitiwa na vikosi vya serikali, lakini muda mfupi baada ya wanajeshi wa serikali kuondoka kwa ajili ya kupishana zamu, magaidi wa al-Shabaab waliuvamia na kuuteka, na sasa uko mikononi mwao.

Naye Abdiasis Abu Musab, msemaji wa al-Shabaab amesema wanajeshi wa serikali walikimbia walipofikiwa na habari kwamba wanachama wa genge hilo la kitakfiri wamesonga mbele na wamekaribia kuudhibiti mji huo.

Uwanja wa Ndege wa Bossaso eneo la Puntland

Amesema, "Jeshi la Puntland lilisikia tunakaribia wakakimbia, wanafahamu kichapo tulichowapa huko nyuma ndio maana wametoroka."

Mwezi uliopita, kundi hilo la kigaidi na ukufurishaji liliteka mji mmoja wa kistratajia karibu na eneo la Baidoa sambamba na kufunga viwanja zaidi ya 30 vya michezo katika mji mkuu Mogadishu; siku chache baada ya mji mwingine wa Moqokori, ulioko yapata kilomita 300 kaskazini mwa mji mkuu Mogadishu kutekwa na kudhibitiwa na genge hilo.

Tags

Jul 20, 2018 14:18 UTC
Maoni