Sep 02, 2018 13:16 UTC
  • Uchaguzi wa bunge waanza Rwanda, RPF yatabiriwa ushindi

Wananchi wa Rwanda wameanza kupiga kura katika uchaguzi wa bunge ambao unatazamiwa kukipa ushindi chama tawala cha Rwanda Patriotic Front (RPF).

Upigaji kura ambao umeanza leo Jumapili unatazamiwa kuendelea kwa siku tatu katika vituo 2,500 vya upigaji kura katika nchi hiyo ndogo ya Afrika Mashariki.

Kuna watu zaidi ya milioni saba waliojiandikisha kupiga kura kuwachagua wajumbe katika bunge lenye viti 80 ambapo, viti 24 ni maalumu kwa wanawake, viwili  ni vya vijana na kimoja cha walemavu.

Wagombea zaidi ya 500 kutoka vyama vitano vya kisiasa na wagombea wanne huru wanashiriki katika uchaguzi huo.

Weledi wa mambo wanatazamia kuwa chama cha RPF cha Rais Paul Kagame kitadumisha wingi wake wa viti bungeni ambapo sasa kina viti 76.

Rais Paul Kagame akipiga kura 

Walemavu na Wanyarwanda wanaoishi nje ya nchi wanapiga kura leo na kesho wabunge 53 watapigiwa kura. Siku ya Jumanne wapiga kura watawachagua wabunge 24 wa kike na wawakilishi wawili wa vijana.

Matokeo ya uchaguzi yamepangwa kutangawa Septemba 16.

Tags

Maoni