Sep 05, 2018 12:00 UTC
  • Rais Ibrahim Boubacar Keïta wa Mali.
    Rais Ibrahim Boubacar Keïta wa Mali.

Rais wa Jamhuri ya Mali, Ibrahim Boubacar Keïta Jumanne iliyopita alikula kiapo cha awamu ya pili ya uongozi wake katika Ikulu ya Utamaduni mjini Bamako huku wimbi la malalamiko na maandamano ya kambi ya upinzani likiendelea kurindima.

Ushindi wa Ibrahim Boubacar Keïta katika uchaguizi wa rais uliofanyika tarehe 12 Agosti nchini Mali ulipingwa na mpinzani wake, Soumaïla Cissé ambaye amekataa kutambua rasmi matokeo ya uchaguzi huo. Kipindi cha pili cha urais wa Keita kimeanza wakati Mali ikisumbuliwa na matatizo makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama. 

Tangu mwaka 2012 Mali ilitumbukia katika machafuko ya ndani na kukabiliwa na mashambulizi ya makundi ya kigaidi hususan katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo. Suala hilo lilikuwa sababu ya kutumwa kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa MINUSMA kwa kifupi ambacho si tu kwamba kimeshindwa kurejesha amani na usalama bali pia mashambulizi ya kigaidi yameongezeka huko Mali katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Suala hilo limewafanya wachambuzi wa mambo wakosoe utendaji wa Rais Ibrahim Boubacar Keïta katika upande wa masuala ya usalama.   

Khalid Dembélé ambaye ni mtafiti wa kituo cha uchambuzi wa masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii cha Crapes anasema: "Wakati Ibrahim Keïta alipuchukua madaraka ya nchi ghasia na machafuko yalikuwa katika eneo la kaskazini mwa Mali pekee, na baada ya kuongoza nchi kwa kipindi cha miaka mitano sasa ghasia na machafuko hayo yamesambaa katika sehemu kubwa ya Mali na yanaelekea kuwa mapigano ya kikabila na kikaumu."

Raia wa kaskazini mwa Mali wamekimbia makazi yao kutokana na ukosefu wa usalama.

Japokuwa serikali ya Mali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na machafuko ya ndani ikiwa ni pamoja na kutia saini makubaliano ya amani na makundi ya waasi wa kaskazini mwa nchi hiyo na kupasisha sheria ya kuzidishwa idadi ya wanajeshi, lakini hatua hizo hazitoshi na mashambulizi ya kigaidi yanaendelea kuchukua roho za watu wasio na hatia. Hata hivyo kwa mara nyingine tena, Keita ameahidi kurejesha amani na utulivu, kuhuisha umoja na mshikamano na kujenga umoja na mapatano ya kitaifa.

Hali ya uchumi wa Mali pia inaripotiwa kuwa mbaya na imewafanya Wamali wengi waishi chini ya mstari wa umaskini. Ursula Mueller ambaye ni mratibu wa misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa anasema: "Raia milioni tano na laki mbili wa Mali wanahitaji himaya na misaada ya kibinadamu."

Hali mbaya ya uchumi unawasumbua raia wa Mali.

Katika hali ya sasa suala la jinsi ya kudhamini mahitaji muhimu ya kimaisha ndilo jambo linalowasumbua raia wa Mali. Ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma ni suala jingine linalozidisha hali mbaya ya kiuchumi nchini Mali. Kutokana na hali hiyo wapinzani wa serikali wanasema kuwa, Keita ndiye anayepaswa kuwajibika kutokana na masaibu yanayowapata wananchi. Hata hivyo Ibrahim Boubacar Keïta anasisitiza kuwa amefanikiwa kukomesha uhalifu unaosababishwa na ufisadi wa kifedha na kuwakingia kifua wahalifu.

Kwa sasa kunaonekana ufa mkubwa baina ya hali ya kimaisha ya wananchi wa Mali na ahadi zilizotolewa na serikali ya Ibrahim Keita ambayo pia inakabiliwa na changamoto kubwa ya malalamiko ya kambi ya upinzani na misukosuko ya kisiasa.      

Maoni