Sep 07, 2018 14:25 UTC
  • AU: Uchaguzi wa bunge la Rwanda ulikuwa huru na wa haki

Mkuu wa Timu ya uangalizi wa uchaguzi ya Umoja wa Afrika Bi. Aichatou Mindaoudou Souleymane, amesema kuwa, uchaguzi wa bunge la Rwanda umefanyika kwa uhuru na haki.

Amesema lengo la timu  hiyo ni kutoa ripoti sahihi au tathmini juu ya kiwango cha uchaguzi huo, ikiwa ni pamoja na kiwango cha kikanda, bara na kimataifa.

Kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyotolewa na tume ya uchaguzi Rwanda, chama tawala cha nchi hiyo RPF kinachoongozwa na Rais Paul Kagame kinaendelea na uongozi wake katika  bunge la nchi hiyo.

Upigaji kura ulianza Jumapili na kumalizika Jumatatu wiki hii katika vituo 2,500 vya upigaji kura katika nchi hiyo ndogo ya  katikati mwa Afrika.

Rais Paul Kagame wa Rwanda akipiga kura

Kulikuwa na watu zaidi ya milioni saba waliojiandikisha kupiga kura kuwachagua wajumbe katika bunge lenye viti 80 ambapo, viti 24 ni maalumu kwa wanawake, viwili  ni vya vijana na kimoja cha walemavu.

Wagombea zaidi ya 500 kutoka vyama vitano vya kisiasa na wagombea wanne huru walishiriki katika uchaguzi huo.

Tags

Maoni