Sep 08, 2018 07:05 UTC
  • Raia 21 wa Nigeria waachiliwa huru kutoka mikononi mwa kundi la Boko Haram

Jeshi la Nigeria limetangaza habari ya kuachiliwa huru raia 21 kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo imesema kuwa, askari wa serikali wamefanikiwa kuwakomboa raia hao waliokuwa wanashikiliwa na kundi hilo, baada ya kufanya uchunguzi na kisha kushambulia eneo walipokuwa wakizuiliwa. Aidha taarifa hiyo imebainisha kwamba, katika operesheni hiyo wapiganaji wa Boko Haram 14 wameuawa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, raia hao 21 walitekwa nyara na wanachama wa kundi hilo siku tatu zilizopita karibu na eneo la Bulka, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Hayo yanajiri katika hali ambayo Alkhamisi iliyopita, kundi la Boko Haram lilishambulia kambi ya jeshi la serikali katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na kuidhibiti baadaye. Katika shambulizi hilo, zaidi ya askari 48 waliuawa. Kundi la kigaidi la Boko Haram lilianzisha mashambulizi yake tangu mwaka 2009 huko kaskazini mwa Nigeria ambapo katika hujuma hizo, zaidi ya watu elfu 20 wameuawa na wengine zaidi ya milioni mbili na laki sita kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.

Tags

Maoni