Sep 11, 2018 07:32 UTC
  • Mamia ya wahajiri wafariki dunia karibu na pwani za Libya

Zaidi ya wahajiri 100 kutoka nchi za Afrika wamefariki dunia katika kipindi cha siku chache zilizopita baada ya boti zao kuzama katika maji ya bahari ya Mediterania karibu na pwani za Libya.

Wahajiri hao waliokuwa wakisafiri kutokea Libya kuelekea nchi za Ulaya walikuwa wameabiri kwenye boti mbili, lakini katikati ya safari boti hizo zilipinduka na kusababisha watu hao kughariki baharini.

Shirika la Kimataifa la Uhajiri lilitangaza mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu kuwa njia ya baharini ya kutoka Libya kuelekea Italia ni njia hatari zaidi kwa wahajiri wa Kiafrika ambapo tangu ulipoanza mwaka huu wa 2018 wahajiri zaidi ya 1,500 wamefariki dunia katika njia hiyo.

Aidha katika kipindi hicho zaidi ya wahajiri haramu 7,000 wamerejeshwa nchini Libya.

Wahajiri kutoka nchi za Afrika wakitumia mitumbwi yenye usalama mdogo kwa safari zao za kuelekea Ulaya

Libya ni kivuko muhimu zaidi kinachotumiwa na wahajiri wa Kiafrika katika safari zao za kuelekea barani Ulaya.

Wafanyamagendo ya binadamu wanaoitumia vibaya hali ya mchafukoge na kuvurugika amani nchini Libya husafirisha kila mwaka kwa ajili ya kuwapeleka Ulaya makumi ya maelfu ya wahajiri haramu kupitia nchi hiyo mkabala na kulipwa kitita kikubwa cha fedha na wahajiri hao. Hata hivyo idadi kubwa ya watu hao hufia njiani kabla ya kufika mwisho wa safari yao.../

 

Tags

Maoni