Sep 11, 2018 10:11 UTC
  • Waba waua watu 18 nchini Zimbabwe

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Afya wa mji mkuu wa Zimbabwe, Harare ametangaza kuwa mlipuko wa magonjwa ya kipindupindu na homa ya matumbo umeua watu wasiopungua 18 katika jiji hilo katika wiki moja iliyopita.

Clemence Duri amesema ugonjwa huo unasambaa kwa kasi katika maeneo ya kusini magharibi mwa Harare na kuongeza kuwa, watu 400 wamelazwa katika hospitali moja ya mji huo baada ya kupatwa na kipindupindu. 

Clemence Duri amesema kuwa maafisa wa serikali ya Zimbabwe wametumwa kusimamia maeneo yaliyoathiriwa na ugonjwa huo na kwamba timu za kukabiliana na janga hilo pia zimepelekwa katika maeneo hayo.

Ugonjwa wa kipindupindu umekuwa ukitokea mara kwa mara katika vitongoji vya kandokando ya jiji la Harare ambako wakazi wake hawapati maji safi ya kunywa na huduma za afya. Maeneo hayo pia yanasumbuliwa na ukosefu wa miundombinu kutokana na kupuuzwa kwa miaka mingi.

Ukosefu wa maji safi unasababisha kipindupindi Zimbabwe.

Nchi ya Zimbabwe iliyoongozwa na Robert Mugabe tangu ilipopata uhuru hadi mwaka jana wakati kiongozi huyo mkongwe alipoondolewa madarakani, ilikumbwa na janga kubwa zaidi la ugonjwa wa kipindupindu mwaka 2008. Wakati huo watu wasiopungua elfu nne walifariki dunia kutokana na kipindupindu na wengine laki moja walipatwa na maradhi hayo. 

Rais Emmerson Mnangagwa aliyechukua nafasi ya Mugabe ameahidi kuirejesha Zimbabwe katika nchi za kipato cha kati hadi kufikia mwaka 2030.

Tags

Maoni