Sep 11, 2018 13:48 UTC
  • Eritrea na Ethiopia zafungua mpaka wa pamoja baada ya miaka 20

Viongozi wa Ethiopia na Eritrea wamefungua mpaka wao wa pamoja kwa mara ya kwanza baada ya kupita miongo miwili; hatua ambayo inatazamiwa kufungua mlango wa kuimarika uhusiano wa kibiashara wa majirani hao wa Pemba ya Afrika.

Maelfu ya wananchi wa nchi mbili hizo wameshiriki sherehe za kufunguliwa mpaka huo wa pamoja, zilizofanyika leo Jumanne katika kituo cha mpakani kilichoko katika mji wa Zalambessa, kaskazini mwa Ethiopia.

Katika sherehe hizo zilizorushwa hewani mubashara na Televisheni ya Ethiopia, raia pamoja na askari wa nchi mbili hizo wameonekana wakipeperusha bendera za nchi zao huku Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed na Rais wa Eritrea, Isaias Afwerki wakiongoza hafla hiyo ya kihistoria.

Siku chache zilizopita, Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika alipongeza juhudi zilizofanyika kwa ajili ya kuondoa hitilafu baina ya nchi mbili hizo.

Ramani inayoonesha mpaka wa Eritrea na Ethiopia

Eritrea na Ethiopia hivi karibuni zilihitimisha rasmi vita baina yao ambavyo vinatambuliwa kuwa mapigano ya muda mrefu zaidi ya kijeshi barani Afrika, yaliyopelekea kuuawa karibu watu elfu 80.

Eritrea ilijitenga na Ethiopia mwaka 1993 baada ya mapigano ya muda mrefu ya kutaka kujitawala.  

Tags

Maoni