Sep 12, 2018 07:39 UTC
  • Uwanja wa ndege wa Tripoli, Libya walengwa kwa kombora

Duru za habari leo asubuhi zimeripoti kuwa uwanja wa ndege wa Tripoli mji mkuu wa Libya umeshambuliwa kwa kombora.

Hadi sasa hakuna ripoti iliyotolewa kuhusu maafa yaliyosababishwa na shambulio hilo katika uwanja wa ndege wa Mitiga huko Tripoli mji mkuu wa Libya, hata hivyo watu walioshuhudia wameeleza kuwa kulisikika sauti za milipuko kadhaa karibu na uwanja huo wa ndege. Duru rasmi katika uwanja huo wa ndege zimeripoti kuwa ndege kutoka Misri kuelekea Tripoli imelazimika kutua katika mji wa Misrata nchini Libya kufuatia shambulio hilo la kombora. Juzi Jumatatu pia watu wawili waliuawa na kumi kujeruhiwa katika shambulio la kundi la kigaidi la Daesh katika jengo la Shirika la Taifa la Mafuta la Libya mjini Tripoli. 

Shambulio la Daesh dhidi ya Shirika la Taifa la Mafuta la Libya 

Mji mkuu wa Libya, Tripoli  na khususan maeneo ya kusini mwa mji huo kwa muda wa karibu siku kumi zilizopita yalikumbwa na mapigano makali kati ya makundi yenye silaha ambayo yalikuwa yakishambuliana katika ngome zao kwa kustafidi na silaha nyepesi, nzito na nyinginezo. Duru za hospitali huko Tripoli Jumanne iliyopita zilitangaza kuuawa watu 78 na kujeruhiwa wengine 313 katika mapigano ya karibuni katika mji mkuu huo wa Libya na vitongoji vyake vya kusini.  

Tags

Maoni