• Wabunge wa upinzani Zimbabwe wasusia hotuba ya Rais Mnangagwa

Wabunge wa kambi ya upinzani nchini Zimbabwe mapema leo wameondoka bungeni na kususia hotuba ya Rais wa nchi hiyo, Emmerson Mnangagwa, ikiwa ni ishara ya hasira zao dhidi ya matokeo ya uchaguzi uliozusha utata wa rais ambayo yalimpa ushindi kiongozi wa chama tawala.

Wabunge wa chama cha Movement for Democratic Change (MDC) kinachoongozwa na Nelson Chamisa walimzomea Rais Mnangagwa alipoanza kusoma hotuba yake kabla ya kususia hotuba hiyo na kuondoka bungeni. Nje ya ukumbi wa Bunge, wabunge wa MDC walikuwa wakiimba nyimbo zinazokishutumu chama tawala cha ZANU-PF. 

Mwenyekiti wa chama cha MDC, Tabitha Khumalo amesema wabunge wa chama hicho hawawezi kuketi na kusikiliza hotuba ya mtu ambaye haheshimu utawala wa sharia. 

Emmerson Mnangagwa

Kiongozi wa chama tawala cha ZANU-PF katika Bunge la Zimbabwe, Pupurai Togarepi ameutaja mwenendo wa wabunge wa kambi ya upinzani kuwa unasikitisha.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC, Nelson Chamisa anadai Kamisheni ya Uchaguzi ya Zimbabwe ilimnyang'anya ushindi katika uchaguzi wa rais uliofanyika Julai 30 mwaka huu. Uchaguzi huo ulikuwa wa kwanza kufanyika Zimbabwe baada ya kiongozi wa siku nyingi wa nchi hiyo Robert Mugabe kuenguliwa madarakani katika kile kinachotajwa kuwa ni mapinduzi ya jeshi ya mwezi Novemba mwaka jana.

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ambaye ametoa wito wa kuwepo umoja na mshikamano kati ya vyama vya siasa kwa ajili ya kujenga upya uchumi wa nchi hiyo, anakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kukomesha hali ya kutengwa Zimbabwe kimataifa na kurekebisha uchumi unaoyumbayumba kutokana na ukosefu wa ajira na uhaba wa fedha za kigeni.

Tags

Sep 18, 2018 14:42 UTC
Maoni