• UN yataka kupokonywa silaha makundi hasimu Sudan Kusini

Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini amesema kuwa hatua ya kwanza inayopaswa kuchukuliwa na pande hasimu nchini humo kwa ajili ya kuonesha mshikamano wao na makubaliano ya mwisho ya amani ni kuweka chini silaha zao haraka iwezekanavyo.

Nicholas Haysom ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, jamii ya kimataifa haitatoa misaada yake ya kifedha kwa Sudan Kusini bila kwanza kusitishwa vita na mapigano nchini humo. Haysom ameongeza kuwa, amani haiwezi kupatikana Sudan Kusini bila ya makundi hasimu kupokonywa silaha.

Kwa upande wake, mkuu wa kikosi cha Umoja wa Mataifa kinacholinda amani Sudan Kusini, Jean-Pierre Lacroix amesema kuwa, kutiwa saini makubaliano ya amani nchini humo ni hatua muhimu ya kukomesha mgogoro unaoingia mwaka wa tano sasa wa nchi hiyo.

Lacroix ameeleza masikitiko yake kutokana na ripoti za kuwepo mapigano ya hapa na pale baada ya pande hasimu kutia saini makubaliano ya mwisho ya amani.

Sudan Kusini ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio dhidi ya kupindua serikali yake. 

Sep 19, 2018 02:47 UTC
Maoni