Sep 19, 2018 14:42 UTC
  • Wanasiasa wa upinzani DRC waendelea kukutana kuelekea uchaguzi mkuu Disemba 23

Viongozi wa upinzani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamekutana nchini Afrika Kusini na kufanya mashauriano na chama tawala cha nchi hiyo ANC wakiongozwa na Moise Katumbi huku vyama vingine vikiwakilishwa na wajumbe mbalimbali.

Huo ni mkutano mwingine wa wapinzani baada ya ule wa juma lililopita mjini Brussels nchini Ubelgiji ikiwa ni moja ya mikakati ya kuelekea uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliopangwa kufanyika nchini humo Disemba 23 mwaka huu.

Hii ni mara ya kwanza chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC kukutana na wapinzani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya  rais Cyril Ramaphosa kuingia  madarakani ambapo upinzani unaona, kuna mabadiliko katika mtazamo wa serikali ya nchi hiyo kuhusu mchakato wa uchaguzi nchini Kongo Kinshasa.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Wajumbe hao wa upinzani watakutana pia na viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC, ambayo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni mwanachama.

Upinzani nchini DRC unaona kuwa SADC ina mchango mkubwa katika kuishinikiza serikali ya rais Joseph Kabila ili iandae na kusimamia uchaguzi huru na wa haki.

Wakati huo huo, Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (CENI) imetangaza kuwa,  imeanza kupokea vifaa vya kupigia kura kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa mwezi Desemba.

Msemaji wa CENI Jean-Pierre Kalamba, amesema vifaa zaidi vinatarajiwa kuwasili nchini humo vikisafirishwa kwa meli na vitapokelewa na maafisa wake katika Bandari za Matadi, Dar-es-Salam Tanzania na Mombasa Kenya.

Maoni