• Chadema wasusia chaguzi ndogo zote nchini Tanzania wakiituhumu NEC kwa kupendelea CCM

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kujiondoa katika chaguzi ndogo zote zilizotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo (NEC) na zitakazofuata kikisema kuwa, tume hiyo inafanya kazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe ambapo amebainisha kwamba, Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC) inafanya kazi ya kuhakikisha chama tawala cha Mapinduzi CCM chini ya Rais John Pombe Magufuli kinashinda kwa kulazimisha matokeo. 

Freeman Mbowe ametangaza kuwa, chama chao hakitashiriki katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Liwale na kata 37 kwa kile alichosema kuwepo mazingira magumu ya kisiasa na kiuchaguzi. 

Rais John Magufuli ambaye serikali yake inatuhumiwa kwamba, inakandamiza demokrasi ya vyama vingi nchini Tanzania

Akiashiria matukio ya hivi karibuni, Mwenyekiti Taifa wa Chadema amesema kuwa, katika uchaguzi wa Ukonga kulikuwa na vituo feki 16 vyenye wapiga kura zaidi ya 7,000 na viliandaliwa mahususi kwa ajili ya kuongeza kura za CCM. "Tulipeleka malalamiko yetu NEC na kwa Msimamizi wa Uchaguzi, lakini hakuna kilichofayika," amesema Mbowe.

Aidha Bwana Mbowe amesema: “Upole na ukimya wa vyama vya upinzani hauashirii woga hata kidogo, yale mawazo ya wenzetu wa Chama Cha Mapinduzi kuamini wana dola na ndiyo wenye nguvu ni kujidanganya, hakuna jeshi linaloweza kuwa na nguvu kuwazidi raia wa Tanzania.

Kadhalika mwenyekiti huyo wa Chadema ameeleza kuwa, vyombo vya habari vya serikali vimekuwa vikitembea na viongozi wa CCM na vimeacha kushughulika na matukio ya kijamii, na kwamba hata Bunge lililokatazwa kuonyeshwa mubashara kwa kisingizio cha kusema watu wafanye kazi, lakini rais anatembea na (Shirika la Utangazaji la Serikali) TBC.  

Sep 19, 2018 14:48 UTC
Maoni