• Miili ya watu 44 yaopolewa Mwanza, Tanzania, baada ya ajali ya kuzama kivuko

Miili ya watu 44 imeopolewa kwenye maji ya Ziwa Victoria baada ya kivuko cha MV Nyerere kilichokuwa kimebeba mamia ya abiria kuzama jijini Mwanza kaskazini magharibi mwa Tanzania.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela amesema kuwa, idadi ya watu waliofariki kwenye ajali hiyo imefikia 44 huku 37 wakiokolewa lakini hali ya baadhi yao ni mbaya na huenda idadi ya vifo ikaongezeka.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, juhudi za uokoaji ziliendelea mpaka majira ya saa mbili usiku hapo jana ambapo zoezi hilo lilisitishwa kutokana na hali ya giza ambayo ilikuwa kikwazo kutekeleza zoezi hilo.

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amesema kuwa, zoezi hilo la uokoaji linatarajiwa kuendelea tena leo asubuhi.

Mv. Nyerere

Akizungumza na waandishi wa habari hapo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi Jonathan Shana, alisema kuwa, kivuko hicho kilizama wakati kikielekea kisiwa cha Ukara na kwamba kiliondoka saa 6 za mchana na kilipinduka saa 8:00 mchana.

Tanzania ina historia ya ajali za vivuko kuzama, kibaya zaidi kuwahi kushuhudiwa kilikuwa mnamo Mei 1996, wakati meli ya MV Bukoba ilipozama  katika ziwa hilo la Victoria na kusababisha vifo vya takriban watu 1000.

Uchakavu wa vyombo vya usafiri wa majini na kupakia abiria na mizigo kupita kiasi, zinatajwa kuwa sababu kuu mbili zinazosababisha ajali za kuzama vyombo vya usafiri wa majini nchini Tanzania.

Sep 21, 2018 04:24 UTC
Maoni