• Idadi ya waliofariki katika ajali ya kivuko Tanzania yapindukia 150

Idadi ya watu waliofariki katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere kwenye ajali ya Ziwa Victoria nchini Tanzania imeongeza na kupindukia 150.

Taarifa zinasema MV Nyerere iliyozama Alhamisi ilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 101 lakini imebainika kuwa ilibeba abiria na mizigo kupindukia kiwango kinachoruhusiwa.

Msemaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzanai Godfrida Jola amenukuliwa akisema kuwa makadirio yanaonyesha zaidi ya watu 200 wamepoteza maisha. Amesema wavuvi na mashuhuda wengine wanasema kivuko hicho kilikuwa kimebeba abiria kupindukia kutokana na kuwa Alhamisi ilikuwa siku ya soko.

Kivuko hicho kilizama wakati kikielekea kisiwa cha Ukara na kwamba kiliondoka saa 6 za mchana na kilipinduka saa 8:00 mchana.

Rais John Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  ameagiza bendera ya taifa ipepee nusu mlingoti kuomboleza tukio hilo.

Maafisa wa usalama wakiwa wamebeba miili kufuatia ajali ya MV Nyerere katika Ziwa Victoria

Aidha ameagiza wote waliohusika na mkasa huo wakamatwe akiwemo kapteni wa kivuko hicho, ambaye taarifa zinasema, tayari amekamatwa kusaidia katika upelelezi. Kadhalika ameagiza kuundwa kwa timu itakayoshughulikia uchunguzi huo. Amewataka wanasiasa kutotumia mkasa huu kama 'kiki za kisiasa' na waache vyombo vya dola vifanye kazi yake.

Tanzania ina historia ya ajali za vivuko kuzama, mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa ikiwa ni ile ya mnamo Mei 1996, wakati meli ya MV Bukoba ilipozama  katika ziwa hilo la Victoria na kusababisha vifo vya takriban watu 1000.  Aidha mwaka 2011 karibu watu 200 walipoteza maisha wakati meli ya MV Spice Islander I ilizama karibu na pwani ya Zanzibar.

Uchakavu wa vyombo vya usafiri wa majini na kupakia abiria na mizigo kupita kiasi, zinatajwa kuwa sababu kuu mbili zinazosababisha ajali za kuzama vyombo vya usafiri wa majini nchini Tanzania.

Tags

Sep 22, 2018 07:46 UTC
Maoni