Sep 22, 2018 16:47 UTC
  • Manusura wa ajali ya kivuko Tanzania: Kapteni alishughulishwa sana na simu na kusababisha ajali

Mchori Bulola, mmoja wa watu walionusurika kwenye ajali ya kuzama kivuko cha MV Nyerere mkoani Mwanza nchini Tanzania amesema kuwa, chanzo cha ajali hiyo kilikuwa mzigo mkubwa ambao kivuko hicho kilikuwa kimeubeba.

Bulola ameongeza kwamba baada ya abiria kuona hali hiyo walimueleza kapteni aliyekuwa akiendesha kivuko hicho lakini hakujali na badala yake akaanza safari. Amezidi kufafanua kuwa, wakiwa njiani walimshuhudia kapteni huyo akiwa anajishughulisha na kuzungumza na simu ambapo ghafla alishtuka na kukuta kivuko kikiwa tayari kimehama kwenye uelekeo wake na hivyo kulazimika kukata kona haraka, jambo ambalo lilisababisha mzigo kuegemea upande mmoja. Kwa mujibu wa Mchori Bulola, kufuatia hali hiyo kivuko hicho kilizama majini na kusababisha ajali iliyoua mamia ya watu.

Mchori Bulola, mmoja wa watu walionusurika kwenye ajali ya kuzama kivuko cha MV Nyerere mkoani Mwanza 

Wakati huo huo, Alphonce Charahani, mhandisi wa kivuko hicho ameokolewa akiwa hai ndani ya maji. Mmoja wa wazamiaji kwa jina la Daniel Kondoyo amesema kuwa, tangu juzi Septemba 20, 2018 kilipozama kivuko hicho walikuwa wakikigonga ili kufahamu iwapo kulikuwa na watu ndani yake ambapo kila walipogonga walisikia mtu mwingine akigonga kwa ndani. Imeelezwa kuwa, Charahani alikuwa amejipaka mafuta ya oili mwilini ambayo wameielezea kuwa husaidia maji yasiweze kupita katika vinyweleo. Katika hatua nyingine ikulu ya Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli imetoa ufafanuzi kuwa siku nne za maombolezi zilizotangazwa jana, sio za mapumziko bali ni za kufanya maombolezo tu.

 

 

 

 

Tags

Maoni