Oct 15, 2018 14:02 UTC
  • Sakata la kutekwa MO Dewji: Familia kutoa Sh1 bilioni kwa atakayetoa taarifa za alipo bilionea huyo

Familia ya bilionea aliyetekekwa nyara nchini Tanzania Mohammed Dewji imevunja ukimya na kusema kuwa, itatoa kitita cha Sh1 bilioni kama zawadi kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazopelekea kupatikana kwa bilionea huyo.

Mwanafamilia na mfanyabiashara maarufu Azim Dewji ambaye pia ni msemaji wa familia hiyo amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kwamba, familia itazichukulia taarifa hizo kuwa kama za siri na pesa hiyo itakuwa zawadi kwa atakayetoa taarifa hiyo itakayyopelekea kupatikana mtoto wao.

Azim Dewji amesema, katika kuhakikisha mtoto wetu mpendwa anapatikana mapema familia tunatangaza donge nono la Tsh bilioni 1 kwa yeyote atakayetoa taarifa muhimu zitakazopelekea kupatikana kwake na taarifa hizo zitakuwa ni siri kati ya mtoa taarifa na familia yetu.

Msemaji wa familia Azim Dewji amesema, mwenye taarifa awasiliane na mwanafamilia Murtaza Dewji kwa namba 0755030014, 0717208478 na 0784783228  na email ya findmo@metl.net.

Aidha Azim Dewji amesema kuwa, tunamshukuru Mwenyezi Mungu na tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na taasisi zake kwa jitihada kubwa wanazozifanya katika kuhakikisha kwamba mtoto wetu anapatikana, vyombo vya habari kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kulichukulia uzito jambo hili na kutoa taarifa kwa umma, taasisi za kidini na zisizo za kidini na kila mmoja wenu kwa maombi ya kutufariji katika kipindi hiki kigumu familia inachopitia.

Muhammad Dewji maarufu kama MO Dewji alitekwa nyara na watu wasiojulikana alfajiri ya Alkhamisi Oktoba 11, 2018 katika Hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam alikokuwa amekwenda kwa lengo la kufanya mazoezi.

Tags

Maoni