Nov 09, 2018 07:51 UTC
  • Kaburi la umati lagunduliwa Ethiopia

Serikali ya Ethiopia imetangaza kugunduliwa kaburi la umati lenye miili 200 katika eneo lililo baina ya maeneo ya Oromia na Somali yanayokumbwa na machafuko.

Wakuu wa polisi wameripoti kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa miili hiyo ni ya watu waliouawa katika mapigano na kundi la wanamgambo wanaojulikana kama Liyu ambao ni watiifu kwa Abdi Mohammed Omer mkuu wa zamani wa eneo la Somali nchini Ethiopia ambaye alilazimishwa kujiuzulu Agosti.  Omer alikamatwa  kufuatia kuibuka ghasia, katika mji mkuu wa eneo la Somali nchini Ethiopia. Kaburi hilo la umati limegunduliwa wakati maafisa wa polisi walipokuwa wakifanya uchunguzi kuhusu jinai ambazo Omer anatuhumiwa kutekeleza katika eneo hilo.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanautuhumu utawala wa Omer kuwa umekuwa ukikiuka haki za binadamu hasa katika jimbo jirani la Oromiya.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Eeneo la Somali nchini Ethiopia kwa muda mrefu limekuwa likikumbwa na uasi wa kundi la Harakati ya Kitaifa ya Ukombozi wa Ogaden. Kundi hilo limekuwa likipigania kujitenga eneo hilo lakini hatimaye mwezi jana waasi hao walitia saini mapatano ya amani na serikali.

Kuenea machafuko nchini Ethiopia kumepelekea serikali mpya ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kukumbwa na changamoto mpya.

Tags

Maoni