Nov 11, 2018 14:20 UTC
  • Utafiti: Mashambulizi ya anga ya Marekani huko Somalia hayana tija

Utafiti mpya umesema mashambulizi ya anga yanayofanywa kila uchao na Marekani nchini Somalia yameshindwa kulitokomeza au hata kulidhoofisha kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab na badala yake yamekuwa na taathira hasi kwa raia wa kawaida.

Utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Hiraal yenye makao makuu yake mjini Mogadishu umebainisha kuwa, Marekani imetekeleza hujuma 27 za anga dhidi ya eti ngome za al-Shabaab, tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, na aghalabu ya mashambulizi hayo yameua idadi kubwa ya raia.

Matokeo ya utafiti huo yametolewa katika hali ambayo, genge hilo la ukufurishaji lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda limeshadidisha hujuma zake. Mashambulizi  ya kigaidi ya siku ya Ijumaa yaliyolenga Hoteli ya Sahafi mjini Mogadishu ambayo hutumiwa zaidi na maafisa wa serikali ya Somalia, yamepelekea kuuawa makumi ya watu.

Taasisi hiyo imetoa mfano hai wa kutokuwa na tija mashambulizi ya anga ya Marekani, kwa kuashiria kuuawa raia wasiopungua 60 wakati Marekani ilipofanya hujuma ya anga mwezi uliopita katika mkoa wa Mudug katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

 

Watu 53 waliuawa katika mashambulio ya kigaidi ya juzi katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu

Kikosi cha Jeshi la Marekani barani Afrika AFRICOM kilitoa taarifa kikidai kuwa shambulizi hilo lililenga maficho ya al-Shabaab. Nayo taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ilidai kuwa shambulio hilo limefanyika katika eneo la Harardhere ambako Marekani inatoa mafunzo ya kijeshi kwa askari wa Somalia, na kwamba makurutu 60 waliuawa kwa 'bahati mbaya'.

Rais wa Marekani Donald Trump mwanzoni mwaka jana 2017 alitangaza kuwa Washington itapanua uwepo wa askari wake nchini Somalia. 

Tags

Maoni