• Watu wasiopungua 18 waaga dunia Kongo baada ya treni kuacha reli

Watu wasiopungua 18 wamepoteza maisha baada ya treni kuacha njia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hayo yalielezwa jana na maafisa husika wa nchi hiyo.

Treni hiyo ilikuwa ikitoka katika mji wa Kindu ikielekea katika mji wa Lubumbashi kusini mashariki mwa nchi ambapo iliacha reli usiku wa kuamkia jana katika eneo la Kasongo. Watu wengine 25 wamejeruhiwa katika ajali hiyo. Rehema Omar afisa wa shirika la reli katika mji wa Samba karibu na ajali ilipotokea amesema kuwa breki zilikataa kufanya kazi wakati treni hiyo ilipokuwa katika mwendo kasi na kusababisha kutoka katika njia yake na kwamba dereva alikimbia baada ya ajali.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

 Wakati huo huo afisa wa huduma za uhamiaji amesema kuwa ameona miili 30 iliyoharibika na mingine chini ya treni hiyo iliyopata ajali. Ilunga Ilunkamba Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema wataalamu wameshafika katika eneo la ajali ili kubaini idadi kamili ya watu waliopoteza maisha na kuchunguza chanjo cha ajali. Ajali kubwa za treni zimekuwa zikitokea mara kwa mara huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  kutokana na kile kinachotajwa kuwa ni kuchakaa kwa mabehewa ambayo ni ya tangu muongo wa 60.

Nov 12, 2018 07:58 UTC
Maoni