Nov 12, 2018 16:22 UTC
  • Mgomo wa matatu Kenya wamalizika baada kutatiza usafiri

Mgomo wa kitaifa wa magari ya abiria yanayojulikana kama Matatu nchini Kenya ulioanza leo umemalizika baada ya kutatiza usafiri na kulazimisha maelfu kutembea kwa miguu.

Wamiliki wa matatu walikuwa wameitisha mgomo kupinga hatua ya serikali kurejesha sheria za barabarani maarufu kama "Sheria za Michuki."

Mgomo huo ulioanza mapema leo Jumatatu uliwalazimisha maelfu ya wasafiri kutembea kwa miguu kwenda maeneo tofauti.

Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya, Dkt Fred Matiang’i, Jumapili ya jana aliwapuuzilia mbali wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma na kusisitiza kuwa msako wa magari mabovu ya uchukuzi wa umma utaendelea ilivyopangwa.

Maafisa wa makundi ya wahudumu wa matatu walikuwa wamelalamikia hatua ya serikali ya kuwataka kutimiza sheria za trafiki maarufu kama “Sheria za Michuki” kufikia Jumatatu na wakatoa wito wa kuwepo mashauriano zaidi kabla ya msako kuanza. Lakini baadaye alasiri wamiliki matatu wamewaomba wananchi radhi na kutangaza kurudia kazini baada ya mkutano wao na maafisa wa Wizara za Usalama na Usafiri.

Gari moshi likiwa limebeba abiria kupita kiasi mjini Nairobi

'Sheria za Michuki' zilianza kutumika 2003 chini ya aliyekuwa waziri wa uchukuzi wakati huo marehemu John Michuki na serikali inasema inazihuisha ili kudumisha usalama barabarani na kuzuia ajali ambazo zimesababisha maelfu ya Wakenya kuaga dunia na wengine kulemaa.

Sheria hizo zilitekelezwa kwa muda mfupi kisha kukajitokeza uzembe uliowapa wahudumu wa magari ya umma uhuru uliosababisha ajali nyingi barabarani na kupelekea idadi kubwa ya watu kupoteza maisha.

Ili kukabiliana na mgomo huo ambao sasa umemalizika, Waziri wa Uchukuzi James Macharia alikuwa ameliagiza Shirika la Reli la Kenya kuongeza safari zake katika mitaa yote ambako linatoa huduma, kama njia ya kuwapunguzia matatizo ya usafiri wakaazi wa Nairobi . Aidha baadhi ya magari ambayo yalipuuza mgomo huo yalitoza nauli zaidi ya mara tatu ya ile ya kawaida.

Tags

Maoni