Nov 13, 2018 14:13 UTC
  • Watu 3 wauawa katika shambulizi la magaidi wa al-Qaeda Mali

Kwa akali raia watatu wa Mali wameuawa huku wanne wa kigeni wakijeruhiwa katika shambulizi la kigaidi lililolenga kituo cha kusafisha madini katika mji wa Gao kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiafrika.

Wizara ya Usalama ya Mali imesema kuwa, gari lililokuwa limesheheni mada za mlipuko liliingia ndani ya kituo hicho saa mbili usiku wa kuamkia leo na kuripuka, na kupelekea kupoteza maisha na kujeruhiwa wafanyakazi hao wa kusafisha madini, ambao walikuwawa wamepewa kandarasi na Umoja wa Mataifa.

Duru za kidiplomasia zimeliambia shirika la habari la AFP kuwa, raia wawili wa Cambodia na mmoja wa Afrika Kusini ni miongoni mwa watu waliojeruhiwa katika hujuma hiyo inayoaminika kufanywa na wanachama wa genge la kigaidi linalohusishwa na mtandao wa al-Qaeda.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, askari wawili wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MINUSMA) waliuawa baada ya kuviziwa na kushambuliwa ghafla na genge moja la kigaidi katikati mwa Mali.

Wanajeshi wa Mali wakishika doria

Nchi ya Mali ilikumbwa na ghasia na ukosefu wa amani baada ya mapinduzi yaliyotokea nchini humo mwaka 2012. 

Mwaka mmoja baadaye, Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MINUSMA) na wanajeshi wa Ufaransa walitumwa nchini humo kwa ajili ya kuwadhaminia usalama raia, lakini vikosi hivyo havijakuwa na utendaji wa kuridhisha katika kurejesha utulivu nchini humo huku vitisho vya ugaidi vikiendelea kuitatiza nchi hiyo. 

Tags

Maoni