Nov 17, 2018 16:33 UTC

Watu wasiopungua 42 wanaripotiwa kuuawa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, kufuatia mapigano kati ya makundi hasimu ya Wakristo na Waislamu.

Duru zinaarifu kuwa mapigano hayo yalianza siku ya Alkhamisi katika mji wa Alindao wakati waasi wa Kikristo maarufu kama Anti-Balaka walipowahujumu Waislamu.

Umoja wa Mataifa umethibitisha vifo vya watu 37 waliokutwa katika mji wa Alindao, ambapo watu 20,000 wameyakimbia makazi yao. Baadhi ya duru zinadokeza kuwa idadi ya waliouawa ni 42 ambapo pia kumetokea uharibifu mkubwa wa mali.

Askari wa kulinda amani nchini CAR

Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo ni miongoni mwa nchi masikini zaidi duniani, ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo François Bozizé kufuatia hujuma ya waasi wa Seleka.

Tangu wakati huo hadi sasa nchi hiyo imekuwa uwanja wa mapigano ya kila uchao kati ya makundi hasimu, hususan lile la Kikristo la Anti-Balaka na kundi la Seleka. Idadi kubwa ya Waislamu wameuawa kwa umati na wengi kulazimika kuwa wakimbizi kufuatia hujuma za genge hilo la Anti-Balaka.

Mwandishi wetu Mossi Mwasi ametuandalia ripoti maalumu kuhusu habari hiyo...

Tags

Maoni