Dec 09, 2018 15:13 UTC
  • Vyama 15 vya siasa Tanzania vyatoa tamko kuhusu muswada wa sheria ya vyama vya siasa

Vyama 15 vya siasa nchini Tanzania kupitia viongozi wake wakuu, vimekutana leo na kutoa tamko la pamoja kuhusiana na muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa uliowasilishwa hivi karibuni na serikali bungeni wakati wa mkutano wa 13 wa bunge la 11 jijini Dodoma.

Vyama vinavyoshiriki mkutano huu ni ACT, CUF, UPDP, DP, CCK, CHADEMA, CHAUMA, NCCR, NLD na ADC.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha CHAUMA, Hashimu Rungwe amesema kuwa, muswada huo unalenga kuwapokonya wanasiasa uhuru wa kufanya shughuli za kisiasa na akawaomba Watanzania wawaunge mkono viongozi hao ili kuzuia muswada huo usipitishwe na kuwa sheria kwa sababu unakiuka katiba ya nchi.

Naye Salum Mwalimu mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa Chadema amesema  kuwa, muswada huo una lengo la kuumaliza upinzani nchini Tanzania kwa kuwanyima wanasiasa haki yao ya kikatiba ya kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kisiasa na kuzungumza na wanachama wao.

Hashimu Rungwe, kiongozi wa chama cha upinzani cha CHAUMA

Kwa upande wake, Zitto Kabwe kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo amesema  kwamba, muswada huo unampa mamlaka makubwa msajili wa vyama vya siasa nchini humo wa kuingilia shughuli za vyama vya siasa, hali ambayo amesema ni kinyume na katiba ya nchi. Zitto Kabwe ameongeza kwamba Watanzania wanaoitakia mema nchi hiyo wanapaswa kuwaunga mkono wanasiasa hao kuukataa muswada huo.

Wapinzani nchini Tanzania wamekuwa wakiituhumu serikali ya Rais John Pombe Magufuli kwamba, inakandamiza demokrasia hasa kutokana na serikali yake kupiga marufuku maandamano na mikutano ya kisiasa ya vyama vya upinzani.

Maoni