Dec 13, 2018 13:57 UTC
  • Ghasia Somalia baada ya kamanda wa zamani wa al-Shabaab kukamatwa

Watu wanne wameuawa nchini Somalia katika ghasia zilizoibuka baada ya kukamatwa aliyekuwa Naibu Kiongozi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab na pia msemaji wa zamani wa genge hilo la ukufurishaji, Mukhtar Robow Abu Mansur.

Nur Ahmed, ofisa wa Tume ya Uchaguzi katika jimbo la Kusini Magharibi ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba, Robow ambaye mwaka jana alijisalimisha kwa jeshi la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, amekamatawa hii leo na wanajeshi wa Ethiopia ambao wako chini ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia, Amisom.

Ofisa mmoja wa Idara ya Intelijensia ya Somalia ambaye hakutaka kutaja jina lake amesema Robow ambaye hivi karibuni alitangaza akiwa mjini Baidoa kuwa atagombea urais wa jimbo hilo katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Disemba 19, amekamatwa na amesafirishwa hadi mji mkuu Mogadishu.

Ingawaje sababu za kukamatwa kwake hazijabainika, lakini mwezi Oktoba mwaka huu, Wizara ya Usalama wa Ndani nchini humo ilisema kuwa, Robow hawezi kuruhusiwa kugombea kiti hicho katika jimbo la Kusini Magharibi kwa kuwa angali chini ya vikwazo vya jamii ya kimataifa ikiwemo Polisi ya Kimataifa Interpol.

Mukhtar Robow, zama zake akiwa msemaji wa al-Shabaab

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, watu wanne akiwemo askari mmoja wa Ethiopia wameuawa katika ghasia zilizoibuka baada ya kukamatawa Robow, kati ya wanajeshi hao wa Amison na watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa kiongozi huyo wa zamani wa al-Shabaab waliokuwa wamejizatiti kwa silaha.

Agosti mwaka jana, Robow alijisalimisha kwa jeshi la nchi hiyo katika mji wa Hudur, kusini magharibi mwa nchi. Kamanda huyo mwandamizi wa zamani wa al-Shabaab alichukua umauzi huo miezi miwili baada ya Marekani kumuondoa katika orodha ya magaidi hatari inaowasaka.

Tags

Maoni