Dec 14, 2018 06:49 UTC
  • Nchi za Afrika zataka msaada wa UN kuituliza Somalia

Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika zimesema zitaomba uungaji mkono wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuiwezesha Tume ya Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kutuliza hali ya Somalia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Monica Juma ameuambia mkutano wa amani wa bara la Afrika mjini Nairobi kuwa, kwa sasa AMISOM inakosa vitu vya kuviwezesha vikosi vyake vya nchi kavu kupambana vilivyo na kundi la kigaidi la Al Shabaab.

Kwa sasa Afrika inawakilishwa na Cote d'Ivoire, Guinea ya Ikweta na Ethiopia kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na wawakilishi hao watatumia ushawishi wao kuhakikisha sauti ya Afrika inasikika kwenye baraza hilo.

Hali baada ya hujuma ya kigaidi iliyotekelezwa na magaidi wa Al Shabab mjini Mogadishu

Bi. Monica Juma amesema, AMISOM haina uwezo wa kutosha wa kuunga mkono operesheni zake katika kupambana na ugaidi nchini Somalia.

AMISOM ina askari wapatao 21,000 nchini Somalia ambao wanalinda amani katika nchi hiyo ambayo imekuwa ikishuhudia vita vya ndani kwa robo karne sasa.

Wanajeshi wa AMISOM walioko Somalia ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone. Nao maafisa wa polisi wa AMISOM ni kutoka Nigeria, Sierra Leone na Uganda. Umoja wa Mataifa umekuwa ukiwafadahili askari hao wa kulinda amani wa nchi za Afrika ambao wana kibarua kigumu cha kukabiliana magaidi wakufurishaji wa Al Shabab ambao mbali na Somalia, huwa wanafanya mashambulizi ya kigaidi pia katika nchi jirani ya Kenya.

 

Tags

Maoni