Dec 14, 2018 07:46 UTC
  • Uchaguzi DRC utaenelea hata baada ofisi za CENI  kuteketea kwa moto

Hata baada ya kuteketea kwa moto ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, CENI kwenye mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Kinshasa, tume hiyo imesisitiza kuwa zoezi la upigaji kura litafanyika katika kipindi cha siku chache zijazo.

CENI inasema kuwa vifaa vya uchaguzi vilivyoteketea kwa moto ni vile ambavyo tu vilikuwa vinalenga wapiga kura wa mji mkuu Kinshasa kwenye uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 23  mwezi huu wa Desemba.

Msemaji wa CENI Jean-Pierre Kalamba amethibitisha tukio hilo la moto kwenye moja ya ofisi za tume hiyo jana Alkhamisi asubuhi. Amesema tume hiyo itatoa tathmini kamili baadaye. Aidha amesema, kwa mujibu wa makadirio, kile ambacho kimeteketezwa hakiwezi kusitisha mchakato wa uchaguzi. Amebainisha kuwa, vifaa vya uchaguzi wa majimbo mengine 25 havikuwepo Kinshasa na vilishahamishiwa majimboni.

Akizungumzia kitendo hicho, cha ofisi kutiwa moto, Felix Tshisekedi, mmoja wa wagombea wa kiti cha urais kupitia chama cha upinzani cha Democracy and Social Progress (UDPS) amekilaani akidai kuwa hofu yake ni kwamba serikali ya DRC itahusisha moto huo na wapinzani wake.

Uchaguzi mkuu wa DRC umepangwa kufanyika Disemba 23 ambapo Emmanuel Ramazan Shadary, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo anagombea kiti cha urais kupitia muungano tawala unaoongozwa na Rais Joseph Kabila.

 

Maoni