Dec 16, 2018 07:40 UTC
  • Marekani: Tuna mpango wa kurejea nchini Libya

Baada ya Marekani kuongoza uvamizi wa NATO uliosababisha uharibifu mkubwa nchini Libya suala ambalo limepelekea watu wengi kuuawa, kamanda mmoja wa jeshi la Marekani, Kanali Adam Chalkley sasa anasema kuwa, hali inayoendelea hivi sasa nchini Libya inatoa fursa ya Marekani kurejesha ubalozi wake nchini humo baada ya kupita miaka sita tangu balozi wa nchi hiyo kuuliwa katika shambulizi lililotokea kwenye ubalozi wake mdogo mjini Benghazi.

Chuki dhidi ya Marekani zimeongezeka sana nchini Libya hasa baada ya Marekani kufanya shambulizi katika eneo la Uwaynat la kusini magharibi mwa Libya karibu na mpaka wa Algeria. Walibya walifanya maandamano makubwa wakilaani shambulizi hilo la Marekani lililoua raia.

Ubalozi mdogo wa Marekani mjini Benghazi Libya ulipochomwa moto tarehe 11, 2012

 

Maandamano hayo yamefanywa na watu wa kabila la Tuareg wanaoishi kwenye eneo hilo lililoshambuliwa na Marekani na waliiomba serikali yenye makao yake mjini Tripoli, ifanye uchunguzi kuhusu mauaji hayo ya kikatili.

Libya ambayo hivi sasa imegawanyika na kukosa utulivu katika kipindi cha miaka saba sasa tangu alipopinduliwa Kanali Muammar Gaddafi.

Itakumbukwa kuwa, mapema mwezi huu wa Disemba, Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Libya ametangaza tarehe ya kufanyika kura ya maoni kuhusu katiba ya nchi hiyo. Emad al Sayeh aliwaambia waandishi wa habari mjini Tripoli kwamba, mchakato wa kura ya maoni kuhusu katiba mpya ya nchi hiyo utaanza katika nusu ya kwanza ya mwezi Februari mwaka ujao wa 2019 na zoezi rasmi la upigaji kura litafanyika kabla ya kumalizika mwezi Februari. 

Maoni