Dec 16, 2018 15:21 UTC
  • Silaha za Israel zinachochea mapigano na mauaji Sudan Kusini

Silaha za utawala haramu wa Israel zenye thamani ya mamilioni ya dola zimeingizwa Sudan Kusini na hivyo kuendelea kuchochea vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimesababisha karibu watu nusu milioni kupoteza maisha.

Gazeti la Jerusalem Post limeandika ripoti inayoonyesha kuwa Israel ina uhusiano wa karibu na utawala wa Sudan Kusini ambao unatuhumiwa kutumia silaha za Israel kuendeleza vita vya ndani ambavyo vimepelekea zaidi ya watu 400,000 kupoteza maisha tokea mwaka 2013.

Taarifa zinadokeza kuwa mkuu wa zamani wa kitengo cha oparesheni cha jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel, Israel Ziv ni mmoja wa madalali waliohusika katika kuiuzuia Sudan Kusini silaha zenye thamani ya mamilioni ya dola. Ziv alitumia shirika la huduma za kilimo Sudan Kusini kama njia ya kuingiza silaha zenye thamani ya dola milioni 150 nchini humo.

Utawala haramu wa Israel uliichochea Sudan Kusini kujitenga na Sudan na imekuwa na uhusiano wa karibu na serikali ya Juba tokea Julai 2011 wakati nchi hiyo ilipojitangazia uhuru.

Rais Kiir wa Sudan Kusini

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.

Nchi hiyo, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake.

 

Tags

Maoni