Dec 17, 2018 02:41 UTC
  • Wanajeshi wa Nigeria wasiopungua 12 wameuliwa katika mapigano na kundi la ISWA

Wanajeshi wa Nigeria wasiopungua 12 wameuliwa na makumi ya wengine hawajulikani walipo baada ya kukabiliana na wanamgambo waliojitenga na kundi la Boko Haram waitwao ISWA huko kaskazini mashariki mwa jimbo la Borno. Hayo yameelezwa na duru za kijeshi za nchi hiyo.

Idadi hiyo ya vifo vya wanajeshi wa Nigeria inatajwa kuwa moja ya idadi kubwa zaidi ya askari waliouawa katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita. Hata hivyo msemaji wa jeshi la Nigeria amesema kuwa idadi hiyo ya vifo iliyotajwa na vyombo vya habari si ya kweli.  Wakati huo huo duru za habari zimesema wanamgambo 28 wa kundi hilo la ISWA pia wameuliwa kwenye mapigano hayo. Mapigano hayo kati ya kundi hilo lililojitenga na Boko Haram na wanajeshi wa Nigeria yamejiri baada ya shambulio la Ijumaa lililofanywa na wanamgambo wa Boko Haram katika eneo la serikali la Gudumbali jimboni Borno ambako kundi lililojitenga na Boko Haram huko magharibi mwa Afrika lijulikanalo kwa jina la ISWA lina ushawishi. 

Kundi la wanamgambo wa ISWA  lililojitenga na Boko Haram

Itakumbukwa kuwa jeshi la Nigeria lilikabiliwa na maafa makubwa mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu wakati wanajeshi wake wasiopungua 100 walipouliwa na wanamgambo wa kundi hilo la ISWA  ambao walishambulia kambi ya jeshi katika eneo la Matele jimboni Borno.

 

  

 

 

 

Tags

Maoni