Dec 18, 2018 07:21 UTC
  • Magaidi 62 wa Al Shabab waangamizwa Somalia

Jeshi la Kitaifa la Somalia limetangaza kuwa magaidi 62 wa Al Shabab wameangamizwa katika oparesheni iliyofanyika kwenye eneo la Gandarsh katika jimbo la Banaadir la kusini mwa nchi hiyo.

Oparesheni hiyo ilifanywa siku za Jumamosi na Jumapili na kuwalenga magaidi wa Al Shabab waliokuwa wanapanga kushambulia kambi ya Jeshi la Kitaifa la Somalia huko  Lower Shabelle.

Wakati huo huo Jeshi la Somalia linapanga kuendesha operesheni ya pamoja na Majeshi ya Umoja wa Afrika nchini humo kwa lengo la kuangamiza kikamilifu magaidi wa Al Shabab katika eneo la Middle Juba.

Hayo yamedekokezwa na Naibu Kamanda wa Majeshi ya Umoja wa Afrika Somalia Charles Tai Gutuai ambaye amesema oparesheni hiyo itajumuisha askari wa Jeshi la Kitaifa la Somalia, askari wa Jimbo la Jubbaland na askari wa Majeshi ya Umoja wa Afrika.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika Somalia

Mwaka 2007 kundi la kigaidi la al Shabab lilijitokeza katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika na kuifanya hali ya Somalia kuwa mbaya zaidi.

Juhudi za kieneo na kimataifa zinafanyika kila leo kujaribu kurejesha amani na utulivu nchini humo. Siku chache zilizopita, nchi wanachama wa Umoja wa Afrika zilisema kuwa, zitaomba uungaji mkono wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuiwezesha AMISOM kutuliza hali ya mambo huko Somalia.

Wanajeshi 21,000 wa AMISOM walioko Somalia ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone. Nao maafisa wa polisi wa AMISOM ni kutoka Nigeria, Sierra Leone na Uganda.

Tags

Maoni