Jan 18, 2019 06:48 UTC
  • Mgomo wa nchi nzima Tunisia katika kumbukumbu ya mapinduzi ya wananchi

Wananchi wa Tunisia wamenza mgomo wa nchi nzima wakitaka nyongeza ya mishahara. Mgomo huo unafanyika katika siku hizi ambapo nchi hiyo inaadhimisha ushindi wa mapinduzi ya wananchi yaliyoiondoa madarakani serikali ya kidikteta ya Zainul Abidin bin Ali mwaka 2011.

Serikali ya Tunis imetangaza kwamba, haina uwezo wa kukidhi matakwa ya wafanya mgomo. 

Tunisia ilikuwa nchi ya kwanza ya Kiarabu iliyoshuhudia kuondolewa madarakani utawala wa kidikteta wa Zainul Abidin bin Ali hapo mwaka 2011 baada ya kutawala nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 33. Maandamano ya wananchi dhidi ya utawala huo yalianza tarehe 17 Disemba na yalimalizika tarehe 14 Januari baada ya dikteta wa zamani wa nchi hiyo kutorokea Saudi Arabia. Mapinduzi hayo ya wananchi wa Tunisia yanajulikana kwa jina la Mapinduzi ya Yasumini.

Tunisia ingali inasumbuliwa na malalamiko ya wananchi dhidi ya serikali licha ya kupita miaka 8 sasa tangu baada ya kuondolewa madarakani utawala wa kidikteta wa Zainul Abidin. Takwimu zanaonesha kuwa, matatizo ya kiuchumi ya watu wa Tunisia yameongeze katika miaka ya hivi karibuni. Deni la nchi hiyo sasa limekuwa sawa na asilimia 70 ya uzalishaji ya ndani wa nchi hiyo. Vilevile tangu mwaka 2011 thamani ya sarafu ya taifa ya Tunisia imeshuka kwa asilimia 60, kiwango cha watu wasio na ajira kimeongezeka kwa asilimia 15 na asilimia 30 baina ya wahitimu wa vyuo vikuu na nakisi ya biashara ya nchi hiyo imefikia karibu dola bilioni 6. Bei ya bidhaa inaendelea kupanda na asilimia 25 ya jamii ya watu wote wa Tunisia haina uwezo wa kujikimu kimaisha. 

Watunisa wanapinga hali mbaya ya uchumi

Hali hii mbaya ya kiuchumi imezusha malalamiko, migomo na maandamano ya mara kwa mwara dhidi ya serikali ya Tunisia. Sasa wafanyakazi laki 6 na 70 elfu wa serikali wameamua kufanya mgomo wa nchi nzima wakidai nyongeza ya mshahara. Mgomo wa sasa umesimamisha shughuli zote za sekta za usafirishaji, afya, elimu na vyombo vya habari.

Tarehe 17 mwezi uliopita wa Disemba Watunisia waliiga harakati ya Vizibao vya Njano nchini Ufaransa na kuanzisha harakati ya Vizibao Vyekundu kulalamikia ukosefu wa ajira, ughali wa bidhaa muhimu, umaskini na ubadhirifu wa mali ya umma serikalini. Lengo kuu na harakati hiyo ya Vizibao Vyekundu limetajwa kuwa ni kurejesha heshima ya Watunisia. Najib al Daziri ambaye ni miongoni mwa wanachama wa harakati ya Vizibabo Vyekundu anasema: Taifa la Tunisia linapigania maslahi ya watoto wake na halitaendelea kuketi chini bila ya kuwa na ajira na kazi. Tumetoa matakwa 22 yanayohusiana na masuala ya kijamii na kiuchumi kama ambavyo harakati ya Vizibao vya Njano huko Ufaransa iliyotoa matakwa 50."

Pamoja na hayo, tofauti na harakati ya Vizibao vya Njano huko Ufaransa, harakati ya Vizibao Vyekundu nchini Tunisia imekhitari njia ya kufanya mazungumzo na serikali lakini wawakilishi wa utawala wa nchi hiyo wamesema waziwazi kwamba, wanapinga suala la kuongeza mshahara wafanyakazi. Waziri Mkuu wa Tunisia, amesema kuwa mgomo wa sasa unaitia hasara kubwa serikali ya Tunis na kuongeza kuwa: Serikali yake haina uwezo wa kuongeza mishahara.

Youssef Chahed

Suala jingine tunalopaswa kuashiria hapa ni kuwa, kwa kutilia maanani hitilafu zilizopo ndani ya chama tawala cha Nidaa Tounes, kuendelea kwa maandamano na migomo nchini humo kunaweza kutoa pigo kubwa kwa Waziri Mkuu wa Tunisia, Youssef Chahed.

Tags

Maoni