Jan 18, 2019 16:05 UTC
  • Wasudan waendeleza maandamano ya mkate, polisi yaua watu watatu

Maandamano ya kumtaka Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan ang'atuke madarakani yameendelea mapema leo Ijumaa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo baada ya mauaji ya watu watatu waliopigwa risasi na polisi katika maandamano ya jana mjini Khartoum.

Maandamano hayo yamefanyika sambamba na mgomo wa madaktari katika hospitali zote za umma nchini Sudan ambao pia wamewataka wenzao wanaofanya kazi katika hospitali za jeshi wasitishe shughuli zao.

Polisi ya Sudan mapema leo imekabiliana na waandamanaji mbele ya hospitali ya katikati ya jiji la Khartoum waliokuwa wakilalamikia mauaji ya watu wawili waliouawa eneo hilo mmoja wao akiwa daktari.

Waandamanaji hao wametoa wito wa kuchukuliwa hatua askari waliohusika na mauaji hayo. Vilevile wametoa nara zinazomtaka Rais Omar al Bashir aondoke madarakani na kulitaka jeshi la Sudan liingilie kati.

Polisi pia wametumia risasi za moto kukabiliana na watu waliokuwa wakisindikiza maiti ya Muawiya Uthman aliyefariki dunia leo baada ya kupigwa risasi katika maandamano ya jana mjini Kharoum.

Wasudan wanamtaka al Bashir aondoke madarakani

Wakari huo huo Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amesema ana wasiwasi mkubwa juu ya ghasia zinazoendela nchini Sudan ambazo hadi sasa zimepelekea kuuawa makumi ya watu na wengine wengi kujeruhiwa.

Taarifa ya Ofisi ya Haki za Binadamu ya UN iliyotolewa Geneva, Uswisi inasema kuwa kuna taarifa za uhakika ya kwamba askari usalama wa serikali ay Sudan wanatumia nguvu kupita kiasi ikiwemo silaha za moto dhidi ya waandamanaji, hali ambayo inatia wasiwasi mkubwa.

Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa, watu wasiopungua 40 wameshauawa katika maandamano hayo yaliyoanza tarehe 19 Disemba 2018.

Tags

Maoni